Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Admeri Hussein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, tokea mwaka jana jeshi hilo limekuwa likifuatilia ajenda ya kufanya mfululizo wa mazoezi ya usalama baharini katika muundo mseto kwa kuzishirikisha nchi za eneo na dunia.
Ameongeza kuwa, katika mazoezi ambayo yameanza Jumanne, Jeshi la Majini limeshafika katika eneo la mazoezi na pia hivi karibuni Jeshi la Majini la India nalo lijatjiunga na mazoezi hayo mseto.
Admeri Khanzadi ameongeza kuwa, sambamba na matukio mazuri yanayojiri katika Bahari ya Hindi, huko Pakistan nako kunafanyika mazoezi ya 'Aman' yenye lengo la kudumisha amani na usalama baharini ambapo manowari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nazo pia zinashiriki katika mazoezi hayo.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hivi sasa kunafanyika jitihada katika Bahari ya Hindi ambazo zinaashiria kuwa nchi za eneo, hasa zenye uwezo mkubwa wa kijeshi baharini, zinashirikiana zaidi kuliko miaka ya nyuma.
Aidha amesema kuwa, nukta hiyo inaonyesha kuwepo ustawi wa usalama kwa maslahi ya usalama wa eneo na biashara ya kimataifa. Admeri Khanzadi amesema kuwa madola ya kibeberu ambayo hadi sasa yamekuwa yakieneza ubabe katika eneo yanapaswa kutambua kuwa yanapaswa kuondoka katika eneo kwani hili ni eneo ambalo lina wenyewe na majeshi ya majini ya eneo yana uwezo wa kutosha wa kudumisha usalama.
342/